Rais wa Mali aliyeondolewa kwa mtutu wa bunduki mwishoni mwa mwezi uliopita, Ibrahim Boubacar Keita jana jioni alifikishwa katika hospitali binafsi, jambo linaloongeza mashaka kuhusu afya ya kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 75, baada ya kuwekwa kizuizini na utawala wa kijeshi unaoshika hatamu ya uongozi wa Mali kwa sasa.
Hata hivyo hali ya afya yake haijaweza kufahamika mara moja na haijaweza pia kuwa wazi kama anaweza kusafirishwa nje ya taifa hilo kwa matibabu zaidi kutokana na mazingira yaliyopo.
Taarifa ya kuwepo kwake hospitali imethibitishwa na shirika la habari la AP kwa kupitia wahudumu wawili wa kituo hicho cha tiba ambao walizungumza kwa masharti ya kutiotajwa majina yao.
Katika picha zake za hivi karibuni rais huyo wa zamani wa Mali alionekana dhaifu, na wasiwasi ukiongezeka tu baada ya kuwekwa kizuwizini katika kambi ya kijeshi ya Kati, nje ya mji mkuu wa Bamako.