Rais aliyepinduliwa wa Niger, Mohamed Bazoum, amewasilisha kesi mbele ya Mahakama ya Haki ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) akitaka aachiliwe huru.
Wakili wa Senegal, Seydou Diagne amethibitisha kwamba kesi hiyo inalenga kumrejesha mteja wake, Mohamed Bazoum, madarakani baada ya kupinduliwa na jeshi Julai 26.
Diagne amesema kuwa mteja wake ametaka utawala wa sasa wa Niger “ulazimishwe kurejesha utawala wa kikatiba kwa kukabidhi mamlaka kwa Rais Bazoum, ambaye atabakia katika nafasi hiyo hadi mwisho wa muhula wake Aprili 2, 2026.”
Wakili Seydou Diagne ameongeza kuwa kesi hiyo, ambayo amewasilishwa mbele ya Mahakama ya Haki ya ECOWAS mnamo Septemba 18, inaushutumu utawala wa kijeshi wa Niger kwa kumkamata rais aliyeondolewa madarakani, mkewe Aziza, na mwanawe Salem “kiholela”, na “kukiuka uhuru wao wa kutembea.”
Kwa mujibu wa wakili huyo, Bazoum, mke wake na mwanawe, ambao wanazuiliwa katika ikulu ya rais tangu baada ya mapinduzi ya jeshi, “ni wahanga wa ukiukaji mkubwa na usiokubalika wa haki za binadamu.”
Viongozi wa mapinduzi ya kijeshi wa Niger wamesisitiza zaidi ya mara moja kuwa Bazoum amekuwa akipata huduma nzuri tangu alipowekwa kizuizini, na kwamba daktari wake anamtembelea. Hata hivyo wametangaza kuwa wanakusudia kumfungulia mashtaka kwa tuhuma za uhaini mkubwa na kudhoofisha usalama wa nchi.