Akihutubia hadhira ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na dunia, rais wa Marekani, Joe Biden, pia alitoa ujumbe kwa dunia kwenda pamoja kutatua changamoto za kidunia licha ya uwepo wa tofauti mbalimbali.
Pamoja na hilo, hotuba yake iligusia msimamo wa Marekani wa hali ya amani na ukiukwaji wa demokrasia barani Afrika.
Amesema taifa lake halitaacha kukemea kusambaa kwa uvunjwaji wa demokrasia na mapinduzi katika eneo la Sahel pamoja na ukanda wa Afrika Magharibi na Kati kwa ujumla.
Katika ajenda muhimu ya mabadiliko ya hali ya hewa, rais Joe Biden, amesema kwamba Marekani imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Amesema ili dunia kuwa salama, lazima ushiriki wa pamoja uwepo kuuokoa ulimwengu na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na kutolea mfano mafuriko ya Libya yaliyo sababisha vifo vya maelfu ya watu. Rais Biden pia alitoa pole kwa wale walioathirika na janga hilo.