Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa atatangaza mabadiliko katika baraza lake la mawaziri siku ya leo Jumatatu, msemaji wa rais, Vincent Magwenya, alisema siku ya jumapili.
Mabadiliko ya baraza la mawaziri yamekuwa yakitarajiwa kwa kiasi kikubwa tangu Ramaphosa kuchaguliwa tena kuwa kiongozi wa chama tawala cha African National Congress (ANC) kwenye kinyang’anyiro cha uongozi wa chama mwezi Disemba mwaka jana, na kumpa nafasi kuwania muhula wa pili mwaka 2024.
Magwenya alisema kwenye kikao na waandishi wa habari na kuongeza kuwa rais huyo alikuwa anasubiri kuapishwa kwa baadhi ya wabunge kabla ya kutangaza mabadiliko hayo.
Rais huyo alitangaza mwezi uliopita kwamba angebuni nafasi ya waziri wa umeme ili kusaidia kutatua mzozo wa kitaifa wa umeme, huku kampuni ya Eskom ikiendelea na mgao wa umeme wenye utata zaidi katika historia.
Rais Ramaphosa anatarajiwa kumteua naibu wa rais mpya baada ya ofisi ya rais kutangaza kujiuzulu kwa David Mabuza kutoka wadhifa huo siku ya Jumatano.