Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasisitiza Watanzania kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kwani masoko yapo.
Mhe. Rais Dkt. Samia amesema hayo leo tarehe 16 Oktoba 2023, wakati akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Mkalama, Mkoani Singida waliojitokeza kwa maelfu kumlaki na kumsikiliza Mhe. Rais Dkt. Samia.
Ameeleza kuwa Serikali inafanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya mazao, hivyo Wakulima Wilayani humo na maeneo mengine wazalishe kwa wingi kwa kuwa masoko ya uhakika yapo.
‘’Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe na timu yake hawalali kutafuta masoko ya bidhaa zetu, kwa hiyo niwahakikishieni limeni masoko yapo, kama soko la nje halipo kwa wakati huo Serikali itanunua yale tulioyazalisha’’, amesema Mhe. Rais Dkt. Samia ambaye yupo katika ziara ya kikazi katika Mikoa ya Singida na Tabora.
Aidha, Mhe. Rais Dkt. Samia alisimama pia katika Mkoa wa Manyara tarehe 15 Oktoba 2023 akielekea kuanza ziara yake Mkoani Singida, ambapo alilakiwa na mamia ya wakazi wa Mkoa huo.