Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika umetoa fursa ya kujadiliana na kubadilishana uzoefu wa njia na mbinu mbalimbali za kuharakisha kufikiwa kwa ufumbuzi wa kukabiliana na changamoto za rasilimali watu nchini Afrika.
Ameyasema hayo leo alipofunga Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasimali Watu (Africa Head of State Human Capital Summit) uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Aidha, Rais Dk.Mwinyi amefafanua masuala mawili ambayo yamejitokeza wakati wa mijadala na michango katika mkutano huo ikiwemo dhana ya kutumia rasimali watu kama nyenzo ya kuongeza kasi ya maendeleo ya jamii kupitia uwekezaji kwa vijana.
Suala la pili amesema utayari wa Afrika kuwekeza katika sekta ya elimu na mafunzo ya stadi za kazi kwa kuwawezesha vijana kuwa na ujuzi ili kufanikiwa.
Mkutano huo umehudhuriwa na Wakuu wa Nchi za Afrika akiwemo Rais wa Kenya Mhe.William Ruto, Rais wa Msumbiji Mhe.Filipe Nyusi, Rais wa Malawi Mhe.Dkt. Lazaraus Chakwera, Rais wa Sierra Leone Mhe.Julius Maada Bio, Rais wa Madagascar Mhe.Andry Rajoelina, Rais wa Sao Tome na Principe Mhe. Carlos Manuel Vila Nova pamoja na Wawakilishi kutoka nchi mbalimbali Afrika.