Rais George Weah wa Liberia anatazamiwa kugombea muhula wa pili katika uchaguzi wa rais unaotazamiwa kufanyika kesho Jumanne.
Weah anatazamiwa kuchuana na wagombeaji wengine 19 katika uchaguzi huo, ambao pia utashuhudia wananchi wa Liberia wakiwachagua wabunge. Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, Waliberia milioni 2.4 wametimiza masharti kushiriki zoezi hilo la kidemokrasia.
George Weah anawania muhula wa pili wa miaka 6 kupitia muungano tawala wa Coalition of Democratic Change (CDC). Wagombe wawili wakuu wanaotazamiwa kumpa ushindani mkali ni Naibu Rais wa zamani, Joseph Nyuma Boakai na mfanyabiashara maarufu Alexander Cummings.
Ingawaje Weah, 57, anasisitiza kuwa kazi kubwa aliyowafanyia Waliberia hasa katika kuboresha sekta ya elimu na kuimarish miundumsingi itamsaidia kushindi kiwepesi muhula wa pili, lakini wakosoaji wake wanahisi kuwa hajafanya mengi tangu aingie madarakani baada ya uchaguzi wa mwaka 2017.
Baada ya kushika rasmi hatamu za uongozi mnamo Januari mwaka 2018, rais huyo wa Liberia aliahidi kupambana na ufisadi ulioenea nchini humo na kuboresha uchumi wa nchi hiyo.