Rais wa Rwanda Paul Kagame amethibitisha kuwania tena kwa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Akihojiwa na gazeti la nchini Ufaransa la Jeune Afrique, rais Kagame amesema yumo miongoni mwa wagombeaji watakaowania uchaguzi huo.
Kiongozi huyo amesema kuwa anafuraha kutokana na namna ambavyo raia wa Rwanda wanaimani naye.
Mnamo mwezi Aprili, rais Kagame alisema kwamba alikuwa anatazamia kustaafu kutoka katika ulingo wa kisiasa baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka 23.
Chama tawala nchini Rwanda, Rwandan Patriotic Front (RPF-Inkotanyi), ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka wa 1998 kilimteua tena rais Kagame kuwa mwenyekiti wake kwa mara nyengine mwezi Aprili.
Kagame amekuwa akiliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki tangu mwaka wa 2000.
Kura ya maoni iliyofanyika nchini humo mwaka wa 2015 iliondoa ukome wa mihula miwili ya kuhudumu kama rais.
Rais Kagame aliibuka mshindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017 kwa asilimia 98.8 ya kura zote.