Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ameituhumu mtandao wa WhatsApp kuwa ni mfumo unaofanya ujasusi, na hivyo amewashauri watu kuachana na WhatsApp na kutumia mitandao mingine.
Akizungumza ikulu mjini Caracas katika mkutano na wawakilishi wa sekta za uvuvi na kilimo za Venezuela, Rais Nicolas Maduro amesema, “WhatsApp iliwapatia walanguzi wa dawa za kulevya wa Colombia orodha ya watu wanaotumia mtandao huo huko Venezuela na kisha walanguzi hao walifanya kazi ya ujasusi kwa miezi kadhaa.”
Rais wa Venezuela ameongeza kusema, mtandao huo wa kijamii ulitumiwa kwa ajili ya vita vya kisaikolojia, kutoa vitisho kwa mamilioni ya viongozi, kuzitishia jamii mbalimbali, viongozi wa serikali za mitaa, familia za wanajeshi na polisi, wanariadha, wasanii na mtu yeyote ambaye hakuunga mkono mapinduzi ya kijeshi na ghasia nchini humo.
Rais Maduro amewatolea wito wananchi kuachana na mtandao wa WhatsApp kwa hiari yao na kujiunga na mitandao mingine. Amewashauri wananchi wa Venezuela kutumia WeChat na Telegram.
Rais wa Venezuela amesema kuwa nchi hiyo imepata mafaniko makubwa sana katika uzalishaji wa kilimo licha ya vikwazo haramu vya kiuchumi vua nchi za Magharibi.