Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli ametaka zoezi la kuhesabu kura katika mchakato wa kura za maoni kuwapata Wagombea nafasi za Ubunge kupitia chama hicho zifanyike kwa uwazi na kwamba huo ndio utakuwa utaratibu kuanzia sasa.
“Waliochukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za Ubunge na Uwakilishi kupitia CCM Tanzania nzima wamefikia 10,367 na katika hao ambao wamekamilisha taratibu zote na kurudisha fomu zao zikiwa kamili ni 10,321 ambao hawakuzirudisha ni 46 tu Nchi nzima” -JPM
“Kiukweli wengi sana wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea Ubunge kupitia CCM, wamefikia 10,367 haijawahi kutokea kwamba katika Chama kimoja wagombea kitu cha Ubunge pekee wanafikia idadi hii, bado Udiwani, nawapongeza sana waliochukua fomu” -JPM
“Kura za maoni zitaanza leo na kesho ni matumaini yangu Viongozi wote watakaosimamia basi watasimamia kwa uwazi bila mizengwe ili mwenye haki na apate haki yake” -JPM
“Ningetamani Viongozi wa Chama changu wakimaliza kupiga kwenye kura za maoni leo na kesho, wafanye kama tulivyofanya Halmashauri Kuu, kura zihesabiwe hadharani, anayepata zero au ngapi ajulikane palepale, uwazi utaendelea kujenga Chama chetu” – JPM