Mwanasiasa wa mrengo wa kushoto Bassirou Diomaye Faye Jumanne amekuwa rais mdogo zaidi wa Senegal, na kuahidi mabadiliko ya kimfumo baada ya miaka mingi ya machafuko na kumtangaza mshauri wake, kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko, kama waziri mkuu.
Faye, 44, hajawahi kushika wadhifa wa kuchaguliwa hapo awali. Alipata ushindi wa raundi ya kwanza kwa ahadi ya mageuzi makubwa siku 10 tu baada ya kuachiliwa kutoka gerezani.
Alikula kiapo cha urais mbele ya mamia ya viongozi na wakuu kadhaa wa nchi za Afrika katika kituo cha maonyesho katika mji mpya wa Diamniadio, karibu na Dakar.
Kisha akarejea katika mji mkuu, huku msafara wake ukilakiwa na mamia ya wakaazi waliojawa na furaha ambao walijipanga kwenye barabara zinazoelekea ikulu ya rais.
Mtangulizi wake, Macky Sall, alimpa Faye ufunguo wa makao makuu ya rais kabla ya kuondoka ikulu.
“Mbele ya Mungu na taifa la Senegal, ninaapa kutimiza kwa uaminifu ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Senegal,” Faye alikuwa amesema mapema siku hiyo.