Aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Jenerali Kale Kayihura, majenerali wengine tisa na maafisa wengine wakuu 99 wameidhinishwa na Rais Museveni kustaafu kutoka jeshini,msemaji wa ulinzi na jeshi Brig Jenerali Felix Kulayigye alisema maafisa hao wakuu 99 wanatoka cheo cha Meja hadi Kanali wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF).
Vyanzo mbalimbali vya habari Ijumaa vilidokeza kwamba maafisa wa mahakama ya jeshi walikutana na kamanda mkuu wa majeshi, Rais Yoweri Museveni kuhusu mashtaka ya jinai aliyoshtakiwa Kayihura.
Mkuu huyo wa zamani wa polisi alishtakiwa kwa kushindwa kulinda vifaa vya vita, kushindwa kuwasimamia maafisa wa polisi, na kusaidia utekaji nyara.
Kayihura amekuwa kwa dhamana tangu 2020 na kumekuwa na ripoti ambazo hazijathibitishwa kuwa Museveni alikubali kufuta mashtaka yote dhidi ya Kayihura.
Jenerali Kayihura, ambaye ni mkereketwa wa vita vilivyomsaidia rais Museveni kuingia madarakani mwaka 1986, kwa wakati mmoja alikisiwa kuwa afisa mwenye mamlaka makubwa zaidi katika jeshi la Uganda.