Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, Zanzibar inaendelea kuleta mageuzi makubwa ya miundombinu kwa lengo la kuwavutia wawekezaji.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 4 Oktoba 2024, Ikulu Zanzibar alipokutana na Rais wa Kampuni ya Samsung C& T Corporation Oh Se-Chul kutoka Korea Kusini na ujumbe wake.
Aidha Rais Dk. Mwinyi amewahakikishia Wawekezaji hao kuwa Zanzibar ina fursa nyingi na kuwakaribisha Zanzibar kuwekeza.
Halikadhalika Dk.Mwinyi ameuelezea ujumbe huo maeneo ya vipaumbele katika uwekezaji hivi sasa kwa Zanzibar ni Utalii, Uchumi wa Buluu, Uvuvi, Usafirishaji na Mafuta na gesi.
Rais Dk. Mwinyi ameipongeza kampuni ya Samsung C&T kwa wazo la kushirikiana na nchi za Afrika hasa za Kusini mwa jangwa la Sahara katika nyanja mbalimbali za uwekezaji pamoja na kuanzisha ofisi yao Tanzania.
Naye, Rais wa Kampuni hiyo Bw. Oh Se-Chul amemuelezea Rais Dk. Mwinyi kwamba Kampuni hiyo katika kutanua wigo wa uwekezaji, kwa sasa imeamua kuja Afrika na Tanzania kuwa kipaumbele kwenye uwekezaji wao pamoja na kufungua ofisi zao hapa nchini.