Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa serikali inahitaji mchango wa wadau mbalimbali kuweza kukabiliana vizuri na mapambano dhidi yavitendo vya udhalilishaji katika jamii, ambavyo vimeonekana kushamiri katika siku za hivi karibuni.
Rais Mwinyi ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa tukio la uzinduzi wa mfumo wa kanzi data (Database system) kwa ajili ya kukusanya takwimu sahihi za mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto katika kongamano la harakati za kutokomeza vitendo vya udhalilishaji Zanzibar.
“Suala hili la udhalilishaji wa wanawake na watoto linawagusa wadau wengi. Zipo taasisi za serikali zinahusika nalo lakini pia zipo taasisi binafsi. Tunahitaji nguvu ya pamoja sote kukabiliana na hili.” Amesema Rais Mwinyi.
Akizungumza pia katika kongamano hilo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility-LSF) nchini Tanzania, Lulu Ng’wanakilala ameiomba Serikali Mapinduzi Zanzibar, iweke mikakati ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia kupitia mijadala na makongamano mbalimbali yanayoandaliwa kwa kushirikisha wadau muhimu wa maendeleo ya jamii visiwani humo.
Ng’wanakilala ameiomba Serikali pamoja na wadau wa kutetea haki za binadamu, watumie fursa ya kongamano hilo, kupata muarobaini wa vitendo hivyo, vinavyoongoza kuathiri kuwanawake.
“Kongamano hili liwe fursa kwa wadau, katika kuweka mikakati thabiti dhidi ya ukatili wa kijinsia,” amesema Ng’wanakilala.
“Ripoti yetu inaonyesha katika kila matukio (4) ya ukatili yaliyoripotiwa na wanawake yalihusisha unyanyasaji wa kijinsia, ambapo visa vyote vilivyoripotiwa vinakadiriwa kufikia asilimia 26.5 kwa mwaka 2020.Hii inaonesha changamoto kubwa ya upatikanaji haki, hasa kwa wanawake wanaokutana na ukatili kwenye shughuli za uchumi na nyumbani,” amesema Ng’wanakilala.