Rais William Ruto wa Kenya amesema yupo tayari kuongea na vijana katika mtandawo wa X, ambao umeibuka kama jukwaa la majadiliano nchini humo kuhusu kampeni dhidi ya uongozi wa Rais Ruto.
“Nasikia vijana wanasema hawataki jukwaa la sekta nyingi.
Labda tuwe na maongezi na Rais kwenye X.
Niko wazi kuwa na majadiliano na vijana kwenye jukwaa ambalo wanafurahia. Ikiwa wanataka nishirikiane nao kwenye X, nitakuwepo,” Rais amesema tarehe 5 au sita majadiliano haya yatafanyika.
Utawala wa Ruto umekumbwa na msukosuko kwa muda wa wiki mbili, huku vijana wa Kenya wakimtaka ajiuzulu.
Maandamano yameongozwa na vijana maarufu Gen Z kwanza wakitaka muswada wa fedha 2024 utupiliwe mbali na sasa wanadai rais ajiuzulu.
Katika mahojiano na waandishi wa habari , rais sasa anataka kufungua ofisi yake kwa vijana, ambao amelalamikiwa kwa kushindwa kuwashirikisha ipasavyo.
“Marafiki wazuri, vijana wa taifa letu, wanangu wa kiume na wa kike walioniunga mkono kushinda uchaguzi nawasikia,” amesema.
“Niliona bwana mmoja wa kijijini kwangu alikuwa anasema ‘rais ametuangusha watoto wengi kijijini hapa hawapati ajira ndio maana wanaenda nje ya nchi.’ Hakujua, rafiki yangu wa kijijini kwangu kwamba wenzake 500 kwa kweli ni sehemu ya mpango wangu kuhusu usafirishaji wa wafanyikazi,” Rais Ruto amesema.
Mpaka sasa KHRC imesema watu 23 wameripotiwa kuuawa kwa risasi au majeraha, katika wiki mbili zilizopita za maandamano katika sehemu tofauti za nchi.