Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu Jijini Dar es salaam leo July 26,2023 ambapo amewataka Viongozi kujiuliza kama Bara walilolirithi kutoka kwa Waasisi waliotafuta Uhuru wa Afrika ndilo Bara wanalotaka kuwarithisha vizazi vijavyo au Wajukuu zao!?, na kusema wakipata majibu watalijenga Bara la Afrika vizuri.
“Bara letu ni Bara lenye Watoto na Vijana wengi, habari hii ni nzuri na pia ni mbaya kwetu, hali hii inaweza kuwa nzuri na yenye tija tukiwekeza kwenye rasilimali Watu kwa kuhakikisha uwepo wa afya bora, elimu bora yenye stadi za maisha ili kujenga nguvu kazi yenye tija kama wenzetu wa Bara la Asia”
“Tusipofanya hivyo hivyo tutaongeza idadi ya Vijana wasio na ujuzi wasioajirika na wa kujiingiza kwenye vitendo viovu na uvunjifu wa amani, sisi tulio hapa tujiulize Bara tulilolirithi kutoka kwa Waasisi wetu waliotafuta Uhuru wa Afrika ndilo Bara tunalotaka kuwarithisha vizazi vijavyo au Wajukuu zetu, je, Afrika tunayoijenga leo ni yenye uchumi endelevu au uchumi unaodumaa?, tukipata majibu hayo tutalijenga Bara letu vema zaidi”
“Nanukuu maneno ya Mwl Nyerere miaka michache kabla ya kufariki wakati akihutubia mkutano Umoja wa Mataifa, NewYork alisema ‘Maendeleo ni Watu, Watu ndio Walengwa, ndio Waanzilishi na Wanufaika wa chochote kinachoitwa maendeleo’ hatuwezi kulikomboa kiuchumi kama hatutoelekeza nguvu zetu kwenye maendeleo ya rasilimali Watu”