Rais Samia Suluhu Hassan amesema Taifa la Tanzania litaendelea kutulia zaidi kwakuwa linaongozwa na Mama ambaye kazi yake ni kulea, kustahimili na kuhakikisha nyumba ina usalama huku akisema Vyama vya siasa vitaendelea kufanya shughuli zao kwa uhuru na kusisitiza kuwa wanaotaka kuandamana wanaruhusiwa na watalindwa.
Haya yamepatikana kwenye video yenye hotuba ya Rais Samia wakati akiongea na Watanzania waishio Ughaibuni (Diaspora Italia) wakati wa ziara yake Nchini humo hivi karibuni ambapo amenukuliwa akisema “Nchi yetu ipo salama, tunaendelea kudumisha amani, utulivu na umoja wa kitaifa, nyumbani kuna umoja usalama na utulivu, kuhusu siasa tunaendelea kudumisha uhuru wa kujieleza na kuhamasisha siasa za kistaarabu zinazolenga kuleta maendeleo ya Watu, tunasisitiza kuvumiliana na kuzingatia sheria ili siasa zetu kisiwe chanzo cha mitafaruku au machafuko”
“Vyama vya siasa vinaendelea kufanya shughuli zao kwa uhuru kabisa, wanaotaka kuandamana tunawaambia ingieni barabarani tutawalinda, wanakwenda weee mpaka wakichoka wanakokwenda wanafika wanafanya yao haya tawanyikeni wanatawanyika, wanaotaka sijui kufanyaje tunawaruhusu, Mtu anatamani kusema tunamwambia kiwanja hiki hapa jukwaa hili, anasema weee akimaliza tunamwambia shuka Baba nenda zako anaenda zake”
“Kwahiyo tunaendelea kutoa uhuru kwa Watu kufanya siasa zao, kuna yale mazoea ya muda mrefu ya siasa za madaraka, kupakana matope na kuzushiana kama zilivyosemwa hapa bado zipo hatukatai bado zipo na nadhani mnazisikia Watu fulani wakisimama hivyo lakini tunaendelea ku-manage”
“Taifa sasa hivi lina Mama na Mama kazi yake kulea, kustahimili na kuhakikisha nyumba ina usalama, kwahiyo Mama yupo katika nafasi ya juu ya Taifa, tutegemee Taifa liendelee kutulia zaidi, jitihada zetu za kuimarisha misingi ya utawala na sheria zinaendelea kutambulika kote Ulimwenguni” – amemalizia Rais Samia.