Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha zaidi ya Sh trilioni 1.4 katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wake ili kutekeleza mradi wa kufua umeme wa maji katika bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) ambao sasa umefikia asilimia 56.
Waziri wa Nishati, Januari Makamba ameiambia kamati ya bunge ya nishati na madini kwamba kasi ya utekelezaji mradi huo imeongezeka kutokana na mikakati kadhaa inayotekelezwa na serikali ikiwemo kumlipa mkandarasi kwa wakati.
Mradi huo wa megawati 2,115 ulianza wakati wa uongozi wa Hayati Rais John Magufuli ambaye (katika kipindi chake) aliidhinisha malipo ya Sh trilioni 2.
‘’Wabunge wa kamati hii wameridhishwa na kufurahia hatua iliyofikia, wamepongeza serikali , wizara na Tanesco na Rais kwa uwezeshaji wake na idhini yake ya kutoa malipo kwa wakati’’ Makamba.
Pamoja na hayo amesema kasi hiyo ya mradi imetokana na mabadiliko ya uongozi na uendeshaji katika mradi huo ili kuhakikisha ubora na viwango vinafikiwa.