Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 7.2 kupitia mradi wa BOOST kujenga shule 12 mpya za msingi na miundombinu mbalimbali katika shule 44 mkoani Ruvuma.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema fedha hizo zimetolewa katika mwaka wa fedha za 2022/2023 na kwamba kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi bilioni 4.34 zimetumika kujenga shule mpya.
Amebainisha kuwa ujenzi wa shule hizo mpya umehusisha ujenzi wa madarasa ya msingi 98,madarasa ya elimu ya awali ya mfano 24,matundu ya vyoo ya elimu ya msingi 136 na matundu ya vyoo ya elimu ya awali 72.
Miundombinu mingine katika shule hizo ameitaja kuwa ni matundu ya vyoo vya walimu 24,vichomea taka 12 na majengo ya utawala 12.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa zaidi ya shilingi bilioni 2.9 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ambayo inahusisha madarasa ya msingi 87,matundu ya vyoo ya msingi 114,madarasa ya elimu ya awali 16,matundu ya vyoo vya awali 48 na nyumba za walimu mbili.
Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Ruvuma Mwl.Edith Mpinzile amesema Mkoa umepokea shilingi milioni 264 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya walimu 12 katika Halmashauri zote nane za Mkoa.