Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelezea masikitiko yake kufuatia kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa ambapo amesema Tanzania imepoteza Kiongozi mahiri aliyejitoa kwa Nchi yake.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa, ameitumikia nchi yetu katika nafasi mbalimbali kwa zaidi ya miaka 35, akianzia ushiriki wake katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbunge, Waziri katika wizara mbalimbali na Waziri Mkuu”
“Tumempoteza Kiongozi mahiri, aliyejituma na kujitoa kwa Nchi yetu, natoa pole kwa Mjane, Mama Regina Lowassa, Watoto (Mheshimiwa Mbunge wa Monduli, Fredrick Lowassa na Wadogo zako), Ndugu, Jamaa, Marafiku na Watanzania wote kwa msiba huu mzito”
“Katika mawasiliano yangu na Familia, nimewaeleza kuwa kama Taifa tuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu, na kamwe wasiache kumtegemea Mwenyezi Mungu na kutafakari neno lake, hasa Kitabu cha Ayubu 1:21, Mwenyezi Mungu amweke mahali pema,
Amina”