Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete kuhakikisha anafanya uratibu wa kuhakikisha Vijana wanapata ajira zinazozalishwa na Sekta mbalimbali hapa Nchini.
Akiongea Ikulu Dar es salaam leo July 26,2024 baada ya kuwaapisha Viongozi mbalimbali, Rais Samia amesema “Mh. Ridhiwani Kikwete umekuwa Naibu Waziri Mtiifu na Bora, umefanya kazi vizuri na kutokana na kazi hiyo tumeona tukupandishe, umekuwa Waziri sasa katika Wizara hiyo ya Vijana na ajira zao na kazi lakini pia una kundi la Watu wenye ulemavu ambapo Viongozi waliokuwepo wamefanya kazi nzuri kiasi na nataka ukasimamie kazi hiyo”
“Kazi yako kubwa kwenye ile Wizara ni uratibu wa kuhakikisha Vijana wanapata ajira zao, kunakuwa na uzalishaji wa kazi katika Sekta nyingine, kilimo, madini, uvuvi kote kuna ajira kwa Vijana, nataka ukawe mratibu na ukahakikishe kila Sekta inatoa ajira kwa Vijana na tukikuuliza Ridhiwani mpaka kufikia December mwaka huu kama tupo January mwakani, tumetengeneza ajira ngapi uniambie kwenye finger tips kisekta, kilimo hizi wapo hizi, ndio kazi yako, kazi yako sio wewe kutengeneza ajira kwa Vijana, kazi yako ni kuhakikisha Sekta zinatengeneza ajira kwa Vijana nawe unaratibu kazi lakini na haki zao”
“Pia ndani ya Wizara yako kuna mifuko ya hifadhi za Jamii, nenda kaisimamie iendeshwe kisayansi, mifuko hii ina fedha za Watu, sio pesa za Serikali ni pesa za Wafanyakazi ambao wanaweka akiba zao za baadaye kwahiyo nenda kasimamie na uhakikishe mifuko hii inakuwa endelevu na haiendi kupotea au kufilisika, pia kasimamie miradi inayotekelezwa na mifuko hii kuna fedha nyingi imeshatumbukia miradi haizalishi kwahiyo nenda kasimamie”
#MillardAyoUPDATES