Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan amempandisha cheo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Camilius Wambura kuwa Kamishna wa Polisi (CP).
Pamoja na kumpandisha cheo, Rais Samia amemteua CP Camilius Wambura kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Kabla ya uteuzi huo, CP Wambura alikuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan amempandisha cheo Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Hamad Khamis Hamad kuwa Kamishna wa Polisi (CP).
Pamoja na kumpandisha cheo, Rais Samia amemteua CP Hamad kuwa Mkuu wa Kamisheni ya Fedha na Lojistiki wa Jeshi la Polisi Tanzania.
Kabla ya uteuzi huo, CP Hamad alikuwa Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Makao Makuu ya Polisi Zanzibar.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ametengua uteuzi wa Bi. Azza Hilal Hamad aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu. Bi. Azza atapangiwa majukumu mengine.
Kufuatia uamuzi huo, Rais Samia amemteua Bi. Prisca Joseph Kayombo kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu. Kabla ya uteuzi huo Bi. Kayombo alikuwa Afisa Mkuu wa Utawala na Utumishi katika Wizara ya Fedha na Mipango na ataapishwa pamoja na Makatibu Tawala wengine siku ya Jumatano tarehe 02 Juni, 2021 Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.