Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya Kitaifa nchini India kuanzia tarehe 8 hadi 11 Oktoba 2023 kufuatia mwaliko wa Mheshimiwa Droupadi Murmu, Rais wa Jamhuri ya India.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa ziara hiyo inafanyika ikiwa ni miaka nane kupita tangu ziara ya mwisho ya Kiongozi wa Tanzania nchini humo.
Mhe. Waziri Makamba amesema ziara hiyo ni muhimu kutokana na historia iliyopo kati ya Tanzania na India kidiplomasia, kiuchumi, kibiashara, kidini, kiutamaduni na Maisha ya India ambayo yapo nchini Tanzania.
Amesema kuwa ziara hiyo inatarajia kuinua ubora wa huduma za Afya nchini ambapo taasisi ya upandikizaji wa figo na kiwanda cha kutengeneza chanjo za wanyama na binadamu zenye ubora vitaanzishwa, kuwezesha ushirikiano mkubwa kati ya Hospitali zetu na Taasisi za India zinazotoa huduma za afya kwa mifumo ya Tiba Asilia pamoja na kuwezesha upatikanaji wa dawa zenye ubora kwa gharama nafuu.
Faida nyingine ni kuinua na kuongeza biashara ya mazao yanayozalishwa nchini hususan mbaazi, kunde, parachichi na ufuta, kuwezesha uwekezaji wa moja kwa moja kwa kuvutia uwekezaji kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa na kampuni mbalimbali kutoka India; kuimarisha Ulinzi na Usalama katika usafiri wa majini ambapo India inatarajia kuanzisha karakana ya utengenezaji wa vyombo vya majini na ukarabati.