Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan leo June 09,2023 amefungua na kushiriki Mkutano wa 14 wa Baraza la Biashara (TNBC), Ikulu Dar es salaam ambapo moja ya mambo aliyoyasema kwenye hotuba yake ni kwamba kazi kubwa inaendelea kufanyika ya kuboresha mifumo ya TEHAMA kwenye Sekta za Umma ili ianze kusomana ambapo ameahidi kuwa sio zaidi ya miezi sita kinachotokea Bandarini atakuwa anaweza kukisoma akiwa Ikulu.
Rais Samia amenukuliwa akisema “Kazi kubwa inaendelea kufanyika ya kuboresha mifumo ya TEHAMA, mifumo yetu haisomani, taarifa hazioani, kazi tunayokwenda kufanya kwa nguvu kubwa sasa ni kufanya mifumo ndani ya Sekta ya Umma isomane pia iwe na vigezo vya Kimataifa”
“Changamoto zilizotajwa hapa hizo za Kariakoo na nini ni kwamba mifumo yetu haijaweza kuchukua taarifa zote hizo, kazi iliyopo sasa ni kuhakikisha mifumo yetu inabeba taarifa zote hizo ili tuweze kuwa na taarifa nyingi ambazo zitapelekwa kufanya maamuzi, hiyo ni kazi mbele yetu kwa upande wa Serikali na ninawaahidi nadhani sio zaidi ya miezi sita tutakuwa tunasoma kinachotokea Bandarini nakisoma Mimi Ikulu huku”