Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi wa Michezo nchini kubadilika ili michezo iendeshwe kwa weledi na kuwataka waache kutegemea kuvuna wasipopanda.
Akiongea wakati wa hafla ya chakula cha mchana na Mabingwa wa Ukanda wa CECAFA kwa Vijana U15 Ikulu ndogo ya Tunguu, Zanzibar, Rais Samia amesema-“Michezo ni biashara kubwa , Viongozi wa Michezo badilikeni ili michezo iendeshwe kwa weledi tuache kutegemea kuvuna tusipopanda na tuweke mipango endelevu kuwekeza kwa Vijana, Mabaraza ya Michezo yaendelee kuratibu na kufuatilia utendaji wa Vyama vya Michezo na kuhakikisha vinaendeshwa na kujiendesha kwa manufaa ya Taifa”
“Ujenzi wa viwanja vya michezo ni gharama kubwa, viwanja vyote vinavyojengwa na kukarabatiwa vitumike kwa uangalifu na vifanyiwe matengenezo uharibifu unapojitokeza badala ya kusubiri uharibifu mkubwa zaidi na hivyo kuongeza gharama maradufu”
“Kuna kipindi nililetewa gharama za kukarabati uwanja wa Taifa nikauliza kwani TFF wako wapi?, wao si wanatumia uwanja?, kwani Watu wanaoingia kule si wanalipa? hiyo pesa iko wapi?, nikawaambia TFF zile pesa kama wameshazitumia wazitafute wakarabati”
“Ni bahati yao tu kwamba tuna mashinadano makubwa kwahiyo tukakarabati lakini msimamo wangu na ambao mitamwambia Rais Mwinyi ni kwamba viwanja vinajichukulia yale mafungu mnayotenga sijui huyu achukue ngapi TFF sijui achukue ngapi, muweke na ya mafungu ya kukarabati kiwanja na sio mnasubiri uwanja umeharibika kisha Serikali mnaipa jukumu la kukarabati”