Serikali kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) itarasimisha makazi yasiyorasmi kwa kutambua, kupanga, kupima na kumilikisha viwanja visivyopungua 27,600 katika kata 7 kwa upande wa mjini na jumla ya mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 90 itaandaliwa wilayani Kyela mkoa wa Mbeya.
Hayo yamebainishwa tarehe 20 Juni 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Kyela Bi. Josephine Manase wakati wa ufunguzi wa kikao cha kujadili utekelezaji wa mradi wa LTIP katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela.
Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi wenye lengo kuu la kuboresha ufanisi katika utawala wa ardhi na usalama wa milki za ardhi utaongeza idadi ya miamala itokanayo na nyaraka za ardhi, kupunguza muda unaotumika kupata nyaraka za umiliki, kuongeza uelewa wa usalama wa ardhi kwa kuzingatia jinsia na kuongeza ufanisi utakaopelekea wamiliki kuridhika na mchakato wa uandaaji wa nyaraka za umiliki.
“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mradi huu utakaopelekea vijiji vyote katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela kuwa na Mpango wa matumizi ya ardhi ambapo hapo awali vijiji 3 kati ya 93 vilikuwa na mpango huo lakini kwa kupitia mradi huu vijiji vyote 90 vilivyobakia vitanufaika kuandaliwa mpango wa matumizi ya ardhi’’ amesema Manase
Aidha, amesema uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi kwa upande wa vijijini pamoja na urasimishaji makazi kwa upande wa mjini utapelekea kupunguza au kumaliza kabisa migogoro ya ardhi katika Wilaya hiyo.
Ametoa rai kwa watendaji wote katika Wilaya hiyo kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha malengo ya mradi yaliyokusudiwa kwa kusaidiana na maafisa kutoka Wizara ya Ardhi wanaotekeleza majukumu hayo.
Mhe. Kefa Oscar Mwanganda, Diwani wa Kata ya Ndandalo wilayani Kyela amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huo kwani utakuwa suluhu ya migogoro ya ardhi na itasaidia kuongeza usalama wa milki za ardhi za wakazi katika maeneo yao.
Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo pamoja na lengo lake kuu la kuboresha ufanisi katika utawala wa ardhi na usalama wa milki za ardhi pia umejikita katika utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya ardhi kwa kuzingatia haki za makundi maalumu kama vile wanawake, vijana, walemavu, wafugaji na wakulima.