Mkutano huo umewakutanisha wakuu wa nchi za Afrika huku Rais Samia Suluhu Hassan akionya juu ya uwekezano wa bara la Afrika kuzalisha vijana watakaokosa matumaini kuhusu bara lao.
Rais Samia aliyefungua mkutano huo katika jiji kuu la kibiashara Dar es salaam amewatahadharisha viongozi wenzake juu ya haja ya kuchukua hatua madhubiti ili kuwasaidia vijana ambao idadi yao inazidi kuongezeka.
Amesema Afrika haiwezi kubaki salama kama mipango na vipaumbele vyake havitaakisi kukwamua changamoto na mahitaji yanayowakabili vijana ambao baadhi yao anasema wamelazimika kutorokea katika nchi za ng’ambo kwa matumaini kustawisha maisha yao.
Rais samia pia amesisitiza haja ya viongozi wa Afrika kuwa na ajenda moja inayozungumza kuhusu kuwastawisha vijana hasa katika wakati huu ambako dunia inaingia katika mapinduzi ya nne ya viwanda.
Uendelezwaji vijana kwa njia ya kuwapatia mitaji, ujuzi pamoja elimu yenye ufanisi ni baadhi ya mambo yaliyowatawala katika hotuba yake iliyofungua mkutano huo ulioanza jana kwa ngazi ya mawaziri.
Sambamba na hayo rais wa Kenya William Ruto alikutana na rais Samia Suluhu Hassan, siku moja baada ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kudai kuwa alipuuza matoleo yake ya upatanishi ya kushughulikia mzozo wa kisiasa wa Kenya wiki mbili zilizopita.