Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wadau wa eneo huru la Biashara Barani Afrika, kufanya tathmini ya maazimo ya Kongamano la kwanza la mwaka 2022 ili kuwasaidia wanawake kuimarika zaidi kibiashara.
Hayo yamesemwa kwa niaba yake na Mhe. Kassim Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa ufunguzi wa Kongamano la pili la Wanawake kwenye Biashara Barani Afrika Desemba 06, 2023 jijini Dar Es Salaam.
Amesema kufanyika kwa kongamano hilo nchini Tanzania kwa mara ya pili ni heshima kwa nchi kwani makongamano kama hayo yanatoa nafasi muhimu kwa wadau hasa wanawake kujadili changamoto zao ikiwemo upatikanaji wa mitaji na mikopo ya masharti nafuu, teknolojia na ukosefu wa taarifa sahihi za fursa na mahali zilipo.
Amebainisha kwamba, maazimio ya kongamano la kwanza yamechangia kwa kiasi kikubwa kwenye uaandaaji wa itifaki ya wanawake na vijana katika biashara na mkataba wa eneo huru la biashara ili kuwawezesha kufanya vizuri zaidi.
“Wakati wa kongamano hili, mfanye tathmini ya maazimio hayo, muweke mikakati endelevu ili kuibua fursa kwa yeyote anayetaka kukua zaidi katika eneo huru la Biashara Afrika.” amesema Mhe. Majaliwa.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akitoa Salaam za Wizara yake, amesema uwezeshaji wanawake na wasichana kiuchumi ni mojawapo ya vipaumbele vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuleta Usawa wa Kijinsia hivyo kufikia maendeleo jumuishi na endelevu.
Dkt. Gwajima amesema, Tanzania imeridhia na inatekeleza Mikataba na Maazimio ya Kikanda na Kimataifa ikiwemo Mkataba wa Eneo huru la Biashara Barani Afrika, ambao unatoa fursa za kiuchumi kwa wanawake na hata wanaume katika biashara ndani la Afrika.