Mvua kubwa za El-Nino zilizonyesha zimeleta athari maeneo mbalimbali hapa Nchini ikiwemo katika Mkoa wa Lindi ambapo zimesababisha uharifu mkubwa wa miundombinu ya barabara na madaraja.
Mvua hizo katika baadhi ya maeneo zilikwamisha shughuli za maendeleo ya Wananchi, na hivyo kuifanya Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kufanya kila linalowezekana kurejesha mawasiliano ya barabara zilizokatika kwa haraka.
Kwa kuliona hilo, Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi bilioni 5 ambazo ni fedha za dharura kwajili ya kurejesha miundombinu ya barabara na madaraja ambayo imeharibika katika Mkoa wa Lindi.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi Mhandisi Emil Zengo ameyasema hayo tarehe 2 Mei 2024; alipotembelea kukagua hatua za ujenzi zinazoendelea katika daraja la Somanga linalounganisha Mikoa wa Dar es Salaam – Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma ambalo lilikatika kutokana na mvua za El-Nino na kusababisha magari ya abiria na mizigo kukwama njiani.
“Tunamshukuru sana Waziri wetu wa Ujenzi Mhe Innocent Bashungwa alitupa maelekezo ya kuhakikisha maeneo yote yaliyoathirika na mvua za El-Nino tuhakikishe ndani ya muda mfupi yanapitika nasi kupitia Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Mohamed Besta tumefanya kazi usiku na mchana kwa sasa miundombinu imerejea” Amesisitiza Mhandisi Zengo
Amewataka Wananchi wanaoishi karibu na barabara kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kwenye kingo za barabara pamoja na kutupa taka ngumu katika mitaro kwani kufanya hivyo kunasababisha maji kushindwa kupita pindi mvua zinaponyesha.
Kwa upande wake Msimamizi Kitengo cha Matengenezo TANROADS Mkoa wa Lindi Mhandisi Robert Mosea ametaja barabara ambazo zimeathiriwa na mvua hizo na zinaendelea na matengenezo ni Kilwa Masoko – Nangurukuru mpaka Liwale, Barabara ya Liwale – Nachingwea, Nachingwea mpaka Kilimarondo pamoja na Barabara ya Tingi – Kipatimo.
“kwa kuzingatia maelekezo ya viongozi wetu tumeweka kambi maeneo mbalimbali kwa ajili ya kurahisha ukarabati wa barabara hizo na kwa sasa Wakandarasi wapo maeneo yaliyoathirika ili kuimarisha zaidi miundombinu”.