Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiwezesha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuupeleka mradi wa Uboreshaji wa Milki salama za Ardhi kwa maeneo ya Vijijini katika Halmashauri saba hapa nchini ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ni miongoni mwake.
Mradi huo una lengo la kumaliza migogoro ya matumizi ya ardhi na migogoro ya mipaka ya vijiji na kutumika kama dira ya matumizi sahihi ya kila kipande cha ardhi ndani ya Halmashauri huku ukitoa njia sahihi za kusimamia utunzaji wa maeneo ya hifadhi za vilele vya milima, misitu na vyanzo vya maji.
Akiongea wakati wa kikao cha Wadau kujadili rasimu ya mpango huo, katika Halmashauri ya Mufindi, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi, Frank Sichalwe ambaye alikuwa ni Mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Linda Salekwa amemshukuru Rais na Serikali huku akitaka Madiwani kutoa ushirikiano kwenye kutoa maoni kwa niaba ya Wananchi.
“Namshukuru Mh Rais kwa kuridhia kusaini mkataba huu na Benki ya Dunia ambao wametupatia zaidi ya Bil 340 ili kupanga matumizi bora, naomba tutoe ushirikiano kadri wasilisho litakavyokuja kwetu, tujue tumebeba Wananchi huko nyuma, Madiwani mpo hapa tunawategemea kutoa maoni yenu mnakaa na Wananchi mnajua kero ya kutokuqa n mpango madhubuti wa matumizi ya ardhi
“Mradi huu ukimalizika haraka utatoa nafasi DED kuandika mradi mwingine kama Vijiji vitabaki ili waje tena, DED wetu mahiri sana, migogoro ya ardhi ni mingi mpango huu utamaliza migogoro, jana tulikuwa sehemu kuna migogoro ya ardhi isiyohesabika mingi sana”
Mpango huu ni wa miaka ishirini (20) ijayo kuanzia mwaka huu 2023 mpaka 2043 ukiwa na Lengo kuu la kusimamia matumizi ya ardhi na kuimarisha ukuaji wa uchumi wa watu wanaoishi katika Halmashauri ya wilaya kwa kuwa na matumizi endelevu ya rasilimali ardhi na kuzingatia uhifadhi wa mazingira.