Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari amewasili nchini Zambia kuanza ziara ya Kitaifa ya siku tatu nchini humo kuanzia leo October 23 hadi October 25,2023 ikiwa na lengo la kujenga ushirikiano kati ya Nchi hizo mbili zenye historia kubwa kiushirikiano.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kenneth Kaunda Jijini Lusaka, Rais Samia amepokelewa na Mwenyeji wake, Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema na Viongozi wengine wa Taifa hilo.
Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba kuhusu ziara hiyo, akiwa nchini humo Rais Dkt. Samia amekubali mwaliko wa kuwa Mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho ya miaka 59 ya Uhuru wa Nchi ya Zambia, yatakayofanyika kesho October 24, 2023, Jijini Lusaka.
Makamba amesema licha ya Rais Dkt. Samia kuwa Mgeni rasmi kwenye siku hiyo muhimu kwa Watu wa Zambia lakini pia keshokutwa October 25,2023 anatarajiwa kuhutubia Bunge tukufu la Nchi hiyo….“Hii ni heshima kubwa na ya kipekee kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwani anakuwa Mgeni mashuhuri wa nne kuhutubia Bunge hilo tangu mwaka 2012, Viongozi wengine waliowahi kuhutubia Bunge hilo ni Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon mwaka 2012, Spika wa Baraza la Shirikisho la Urusi, Valentina Matvienko mwaka 2018 na Rais wa Italia Sergio Matarella 2022”