Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiwezesha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuupeleka mradi wa Uboreshaji wa Miliki salama za Ardhi kwa maeneo ya Vijijini katika Halmashauri saba hapa nchini ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ni miongoni mwake.
Mradi huo una lengo la kumaliza migogoro ya matumizi ya ardhi na migogoro ya mipaka ya vijiji na kutumika kama dira ya matumizi sahihi ya kila kipande cha ardhi ndani ya Halmashauri huku ukitoa njia sahihi za kusimamia utunzaji wa maeneo ya hifadhi za vilele vya milima, misitu na vyanzo vya maji.
Akiongea leo wakati wa kikao cha Wadau kujadili rasimu ya Mpano huo, katika Halmashauri ya Mbinga, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbinga, Pendo Ndumbaro ambaye alikuwa ni Mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Aziza Mangosongo amesema Mpango huu itapendeza ukiweka maeneo ya kimkakati ya uwekezaji kutokana na rasilimali zilizopo ndani ya Halmashauri ya wilaya ya Mbinga.
“Tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kunufaika na Mradi huu, moja ya vipengele muhimu wakati wa utekelezaji wa mradi huu ni Kuandaa Mpango wa Matumizi ya ardhi ya Halmashauri ya wilaya ambao umekwisha andaliwa Rasimu na sasa ni zamu yetu kama wadau muhimu wa maendeleo ya Halmasahuri ya wilaya ya Mbinga kupitia mpango huu na kutoa maoni yetu”
Mpango huu ni wa miaka ishirini (20) ijayo kuanzia mwaka huu 2023 mpaka 2043 ukiwa na Lengo kuu la kusimamia matumizi ya ardhi na kuimarisha ukuaji wa uchumi wa watu wanaoishi katika Halmashauri ya wilaya kwa kuwa na matumizi endelevu ya rasilimali ardhi na kuzingatia uhifadhi wa mazingira.