Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameagiza kusimamishwa kazi kwa uongozi wa Soko la Kariakoo, Jijini Dar es Salaam na vyombo vya serikali vifanye uchunguzi wakati serikali inafanya tathimini ya soko hilo.
Rais Samia ametoa agizo hilo alipofanya ziara katika soko la Kariakoo ambapo amesema serikali itafanya tathimini katika soko hilo kwani hali iliyopo ndani na nje ya soko hilo binafsi haikumridhisha.
“Wakati tunaendelea kufanya tathimini naomba nimuagize na naambiwa Waziri wa TAMISEMI alitoa hayo maagizo kusimamisha uongozi uliopo tutaangalia mpaka ngazi gani na tuwatake vyombo vya serikali vifanye uchunguzi kwanza halafu tutakuja kutoa maamuzi,” Rais Samia.
“Kuanzia wakati mpendwa wetu Dk. Magufuli yupo hadi leo lengo letu ni kusaidia wafanyabiashara wadogo, tuliyoyaona ni kama usaidizi wa wafanyabiashara wadogo haupo, maamuzi yangu tutafanya tathimini ya uendeshaji wa soko na tuone kama hili soko lisimamiwe na uongozi uliopo au Jiji lichukue hili soko, “ Rais Samia.
“Wakati serikali inawabeba na nyinyi jitahidini kufuata sheria zinazowekwa katika maeneo mlipo, nimeona vibanda kila pahali nitakaa na viongozi wa Jiji tuone njia nzuri ya kuwapanga na kugawa maeneo ya kazi,” Rais Samia.