Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (Common wealth), unaotarajiwa kufanyika Zanzibar, kuanzia Tarehe 4 hadi 8, machi mwaka huu huko Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege.
Ameyasema hayo Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi na Utawala Bora Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Amesema Tanzania imepata heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Jumuiya ya Madola na takriban miaka 10 iliopita sasa ni mara ya kwanza kufanyika Mkutano huo Tanzania ambao utahudhuriwa na Wageni zaidi ya 300.kutoka nchi 56 Wanachama wa Jumuiya ya Madola.
Balozi huyo ameishukuru Dunia kwa kuichagua Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na sifa na vigezo vya amani na utulivu wa nchi ikiwa ni moja ya vivutio vikubwa vya utalii katika pande mbili zote za Muungano wa Tanzania.
Aidha amesema Tanzania unaendelea kuwa mfano wa utawala bora kupitia muhimili wa Mahakama hasa katika utawala wa sheria, kwa Wananchi kupata huduma mbalimbali za kisheria hasa kwa Watoto.
Mbali na hayo amesema Agenda ya Tanzania ni masuala ya haki kwa Watu na kuitaka Tanzania iwe ni sehemu ya Amani, ili Watu waishi kwa kufuata Sheria za nchi na utaratibu maalumu pamoja na kuwa Mabalozi wazuri kwa kuwatetea wengine wasiyofanyiwa haki ili waweze kupata haki zao.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Haroun Ali Suleiman amesema Mkutano huo utaipatia Zanzibar heshima kubwa kiuchumi,Kisiasa na kijamii jambo ambalo litaweza kuleta tija kwa Taifa.