Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa wachimbaji mkoani Simiyu kufuatia vifo vya zaidi ya wachimbaji 21 waliofukiwa na kifusi katika kijiji cha Ikinabushi,wilayani Bariadi-Mkoa wa Simiyu.
Salamu hizo zimetolewa leo kijijini Ikinabushi wilayani Bariadi-Simiyu na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde wakati akizungumza na wachimbaji katika eneo hilo na kuwasilisha salamu za pole za Rais Samia kwa ndugu,jamaa wa familia zilizopoteza wapendwa wao kufuatiwa kufukiwa na kifusi wakati wa zoezi la uchimbaji.
Mavunde amesema eneo hilo la uchimbaji kwa sasa litasimama shughuli za uchimbaji mpaka Wizara kupitia kitengo cha ukaguzi Migodi na Mazingira kitakapojirdhisha juu ya usalama wa eneo hilo kiuchimbaji ndipo itaruhusu shughuli hizo ziendelee.
Pia, kufuatia maombi ya wachimbaji hao zaidi ya 500 kuomba kuendelea na uchimbaji wa eneo hilo kwa lengo la kujitafutia riziki Rais ametoa maelekezo kwa Wizara kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa ili wachimbaji hao warasimishwe na kupatiwa leseni ya madini.
Katika hatua nyingine, Mavunde amewataka wachimbaji hao waunde kikundi cha pamoja ili kupatiwa leseni na kuzitaka mamlaka za Mkoa na wilaya kusimamia zoezi hilo.
Akizungumza katika mkutano huo,Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mhandisi Andrea Kundo ameishukuru serikali kwa kuwakimbilia kwa uharaka kutokana na majanga yaliyotokea na pia kutumia fursa hiyo kumshukuru Rais kwa hatua ya upatikanaji wa leseni kwa kuwa wananchi hao shughuli yao kubwa ya kiuchumi ni uchimbaji na ndio maisha yao.