Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Jukwaa la Kodi kitaifa lililoandaliwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji pamoja na Sekta Binafsi linalotarajiwa kukutanisha wadau mbalimbali wa kodi.
Hayo yameeelezwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bw. Elijah Mwandumbya, alipokutana na kuzungumza na waandishi wa Habari jijini Arusha, katika ukumbi wa Hazina Ndogo, kuhusu Jukwaa la Kodi na Uwekezaji Kitaifa 2024 linalotarajiwa kufanyika tarehe 27 – 28 Februari, 2024, katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
‘’Serikali imeshirikisha Sekta Binafsi katika hatua zote za maandalizi ikijumuisha ziara za Kikanda ambazo zilifanyika kuanzia tarehe 20 Novemba, 2023 hadi tarehe 07 Desemba, 2023 katika Kanda za Kaskazini (Arusha), Kanda ya ziwa (Mwanza na Shinyanga), Kanda ya Magharibi (Kigoma), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), na Kanda ya Kusini (Mtwara)’’, alisema Bw. Mwandumbya.