Sri Lanka imetangaza hali ya dharura baada ya Rais Rajapaksa na mke wake kukimbilia nchini Maldives, saa chache kabla ya kufika kwa muda wake wa kuachia ngazi. Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe aliyetangaza nia ya kujiuzulu sasa anakuwa kaimu rais.
Saa kadhaa baada ya Rais Gotabya Rajapaksa kuikimbia Sri Lanka mapema leo, ofisi ya waziri ilitagaza hali ya dharura. Licha ya kutangazwa hatua hiyo maelfu ya waandamanaji waliendelea kumiminika katika ofisi ya waziri mkuu Ranil Wickremesinghe, ambaye hivi sasa ndiye kaimu rais, wakimtaka ajiuzulu, huku polisi ikijibu kwa kufyetua gesi ya kutoa machozi.
Msemaji wa waziri mkuu Dinouk Colombage amesema waziri mkuu kama kaimu rais ametangaza hali ya dharura kote nchini humo na kuweka marufuku ya kutembea usiku katika mkoa wa magharibi.