Rais Vladimir Putin amechaguliwa tena kwa 87% ya kura katika uchaguzi wa rais nchini Urusi, kulingana na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo. Matokeo haya ambayo bado niya muda yalitolewa kwa msingi wa kura kutoka 80% ya vituo vya kupigia kura zlizohesabiwa.
Kama inavyotarajiwa katika uchaguzi huu bila mashaka, mkuu wa Kremlin anaelekea kupata ushindi kamili bila upinzani wowote.
Vladimir Putin amewashukuru Warusi kwa kupiga kura katika uchaguzi wa rais ambao ameshinda kwa kiasi kikubwa, kulingana na matokeo ya awali. Rais wa Urusi amebaini kuwa matokeo ya kwanza ya uchaguzi wa rais nchini Urusi yaliyompa ushindi wa wazi yalionyesha “imani” ya Warusi katika utawala wake.
“Tuna kazi nyingi madhubuti na muhimu za kukamilisha. Matokeo ya uchaguzi yanaonyesha imani ya raia wa nchi na matumaini yao kwamba tutafanya kila kitu kilichopangwa,” amesema katika hotuba yake iliyopeperushwa kwenye televisheni usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu.
Vladimir amehakikisha kwamba nchi yake haitajiruhusu “kutishwa” au “kukandamizwa”.