Afrika Kusini itaandaa uchaguzi wa kitaifa na wa majimbo Mei 29, sambamba na siku ya kusherehekea miaka 30 ya uhuru na demokrasia, kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya rais ambao imesema hatua hii imeafikiwa baada ya mkuu wa nchi rais Cyril Ramaphosa kushauriana na tume ya uchaguzi kuhusu tarehe hiyo.
Rais pia ameitisha kikao na wakuu wote wa mikoa na tume kujadili matayarisho ya uchaguzi huo.
Wapiga kura watakuwa wanatarajiwa kuwachagua wabunge wapya wa kitaifa pamoja na bunge la mkoa katika kila jimbo kati ya majimbo tisa nchini humo.
Rais Ramaphosa anawania kuongoza Afrika Kusini kwa muhula wa pili.
Chama chake cha African National Congress kinakabiliwa na ushindani mkali katika uchaguzi huo, huku kura za maoni zikionyesha kuwa chama hicho kinaweza kupoteza umaarufu wake kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30 ya demokrasia nchini Afrika Kusini.