Chama tawala cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Union for Democracy and Social Progress (UDPS) kilithibitisha kugombea kwa Félix Tshisekedi katika uchaguzi wa urais wa 2023 katika kongamano mjini Kinshasa siku ya Jumamosi.
Chama hicho pia kilimpigia kura Tshisekedi kama kiongozi wao kwa miaka mitano ijayo.
Tshisekedi, ambaye amekuwa mamlakani tangu Januari 2019, alikuwa amethibitisha mapema kwamba atawania tena kiti hicho.
Kwa uchaguzi wa wabunge wa kitaifa pekee, UDPS imesimamisha wagombea 495 kwa viti 500 vilivyopo. Kwa uchaguzi wa ubunge wa majimbo, chama kinapendekeza wagombea katika majimbo yote.
Mnamo Desemba, Félix Tshisekedi atachuana na wagombea kadhaa, akiwemo Moïse Katumbi.
Mshindani wake mkuu ambaye ni kiongozi wa chama cha upinzani Martin Fayulu alisema hatagombea iwapo mabadiliko sahihi hayatafanywa kwenye tume ya sasa ya uchaguzi.
Hivi karibuni Human Rights Watch iliishutumu serikali ya Tshisekedi kwa “kukandamiza” na “kutisha” upinzani, miezi minne kabla ya uchaguzi wa rais.
Kundi hilo lenye makao yake makuu mjini New York lilitoa mfano wa Ofisi ya Pamoja ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ambayo imebainisha “vurugu za kisiasa na uchaguzi, kukamatwa kiholela na kuwekwa kizuizini, utekaji nyara na vitisho vinavyolenga wapinzani wa kisiasa.”
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inajitahidi kuzima uasi wenye silaha unaofanywa na waasi wa M23, ambao Kinshasa na serikali kadhaa za Magharibi zinasema kuwa inaungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda.