Spika wa Bunge la Ghana amesitisha uidhinishaji wa mawaziri wapya, na hivyo kuzidisha mzozo kuhusu kucheleweshwa kusainiwa kwa mswada wa kupinga LGBTQ+ na Rais Nana Akufo-Addo.
Mswada huo, ambao unalenga kuharamisha uhusiano wa mashoga na usaidizi kwao, ulipitishwa mwezi uliopita lakini umekabiliwa na changamoto za kisheria. Ofisi ya rais imeomba Bunge lijizuie kutuma mswada huo ili kuidhinishwa na rais hadi changamoto hizo zitakapotatuliwa.
Spika Alban Bagbin amekosoa msimamo wa kiti cha urais kuwa ni “dharau,” akisisitiza kuwa unadhoofisha mamlaka ya bunge. Rais Akufo-Addo anakabiliwa na shinikizo ndani ya nchi, ambapo Waghana wengi wanaunga mkono mswada huo, na kimataifa, huku wafadhili wa nchi za Magharibi na mashirika ya haki za binadamu yakimtaka asitie saini kuwa sheria.
Kucheleweshwa kwa kutiwa saini kwa mswada huo kumezua mzozo wa kisiasa, huku wakili akipinga kupitishwa kwake katika Mahakama ya Juu kwa misingi ya kutotosha akidi ya wabunge wakati wa upigaji kura.
Katika barua aliyoiandikia Bunge hivi majuzi, katibu huyo wa rais aliteta kuwa haitakuwa sawa kwa rais kupokea mswada huo hadi mahakama ifikie uamuzi kuhusu suala hilo. Kwa kujibu, Spika Bagbin amezuia idhini ya mawaziri wapya, na hivyo kuongeza shinikizo kwa rais kuchukua hatua.