Rais wa Iran Ebrahim Raisi anataka kuweka sheria kali kwa wanawake kwa makosa ya hijab (hijabu) licha ya maandamano makali nchini humo. Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la Ujerumani dpa siku ya Jumapili (Aprili 21), Rais Raisi alisema kuwa kuheshimu vazi la Hijabu sio tu ni jambo la kidini bali pia ni wajibu wa kisiasa na kisheria kwa wanawake wa Iran.
Rais aliongeza kuwa hakuna shaka yoyote kwamba ukaguzi lazima uendelee kutekelezwa mara kwa mara.
Matamshi ya rais yamejiri zaidi ya mwezi mmoja baada ya polisi na walezi wa maadili nchini Iran kwa mara nyingine tena kuzidisha msako mkali dhidi ya ukiukaji wa hijabu.
Video kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha mapigano kati ya wanawake na walinzi wa maadili wakati wa ukaguzi.
Kifo cha mwanamke wa Kikurdi wa Iran Mahsa Amini akiwa chini ya ulinzi wa polisi mnamo Septemba 2022 kilisababisha maandamano nchini kote dhidi ya utawala wa Kiislamu na kanuni zake za mavazi.
Amini alizuiliwa na polisi wa maadili kwa sababu ya hijabu inayodaiwa kutokwenda vizuri.
Siku chache baadaye, alifariki katika kituo cha polisi, ikidaiwa kuwa ni matokeo ya vurugu za polisi.