Shirikisho la Soka la Uturuki (TFF) lilisema Alhamisi bodi yake ya nidhamu imepiga marufuku ya kudumu kwa rais wa klabu ya Ankaragucu Faruk Koca kwa kumpiga ngumi mwamuzi baada ya mchezo uliochezwa wiki hii kwenye ligi kuu ya soka nchini humo.
Bodi ya TFF pia iliamua kuwa klabu ya Ankaragucu inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Uturuki italipa faini ya lira milioni mbili ($69,000) na itacheza mechi tano za nyumbani bila mashabiki kutokana na machafuko yaliyohusisha mashabiki na viongozi wa klabu hiyo.
Maafisa wengine mbalimbali wa Ankaragucu walipokea marufuku, tahadhari na faini kuhusiana na tukio la Jumatatu.
Mwishoni mwa mechi yao ya nyumbani dhidi ya Rizespor, Koca waliingia uwanjani na kumpiga ngumi ya uso mwamuzi Halil Umut Meler baada ya Rizespor kufunga bao la kusawazisha dakika ya 97 katika sare ya 1-1. Meler kisha alipigwa teke akiwa amelala uwanjani.