Marekani imeanza kutuma msaada wa kijeshi kwa Israel na silaha mpya siku ya Jumapili, na kuisogeza meli yake kubwa ya kikosi cha wanamaji na angani karibu na Bahari ya Mediterania, kuashiria uungaji mkono wa haraka kwa mshirika wake wa kihistoria kufuatia mashambulizi ya Hamas kutoka Palestina.
Katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Jumapili, rais Joe Biden ametangaza kwamba “msaada wa ziada kwa wanajeshi wa Israel sasa uko njiani kuelekea Israel, na mengine zaidi yatafuata katika siku zijazo,” kulingana na taarifa ya Ikulu ya White House.
“Rais ameagiza uungwaji mkono zaidi kwa Israel kufuatia shambulio la kigaidi la Hamas ambalo halijawahi kushuhudiwa,” serikali ya Marekani imesema katika taarifa yake fupi.
Matangazo maalum zaidi yanawezakutolewa baadaye, Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken alisema hapo awali.