Rais wa Marekani Joe Biden ataondoka Washington Jumanne jioni (Okt 17) kukutana na viongozi wa Israel, Jordan, Misri na Palestina wakati akianza safari yake ya Mashariki ya Kati kwa nia ya kutuliza hali katika Ukanda wa Gaza.
Siku ya Jumatano, Biden atakutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Tel Aviv kwa mazungumzo. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken, tayari amefanya safari mbili nchini Israel tangu shambulio la Hamas tarehe 7 Oktoba.
Baadaye, Biden anatarajiwa kuruka hadi Amman nchini Jordan kwa mazungumzo kuhusu kuharakisha usaidizi wa kibinadamu huko Gaza, ambako atakutana na Mfalme Abdullah wa Jordan, rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi, na rais wa Palestina, Mahmoud Abbas.
Kwa mujibu wa Reuters, msemaji wa usalama wa taifa wa White House John Kirby alisema: “Ataweka wazi kwamba tunataka kuendelea kufanya kazi na washirika wetu wote katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na Israel, kupata usaidizi wa kibinadamu na kutoa aina fulani ya njia salama kwa. raia watoke nje.”