Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, amesema mashambulizi ya kijeshi dhidi ya al-Shabab yanalenga kuliondoa kundi lenye uhusiano na al-Qaeda katika muda wa miezi mitano ijayo.
Waandishi wa habari wanasema ahadi ya kuliondoa kundi hilo ni matumaini makubwa ikizingatiwa kuwa kundi hilo limekuwepo tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, na limejikita katika jamii na kubadili mbinu zake kukabiliana na shinikizo la majeshi ya kimataifa.
Hata hivyo maelfu ya wanajeshi wa serikali wamekuwa wakikusanyika katika mji uliopo katikati mwa Somalia ili kushiriki katika kampeni mpya ya kijeshi dhidi ya kundi hilo la jihad.
Wakati wa awamu ya kwanza ya mashambulio hayo, ambayo yalianza mwaka mmoja uliopita, jeshi na wanamgambo wenye misingi ya koo walifanikiwa kuyateka maeneo mengi kutoka kwa Al Shabab.
Al-Shabab ambayo ina maana ya “vijana”, kwa lugha ya Kiarabu, liliibuka kama tawi la vijana wenye itikadi kali la Muungano wa Mahakama za Kiislamu wa Somalia, ambao uliudhibiti mji mkuu Mogadishu mwaka 2006, kabla ya kulazimishwa kuondoka nje na vikosi vya Ethiopia.