Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu Uchumi Kanda ya Tanga katika Shauri la Uhujumu Uchumi Na. 1 la mwaka 2020 leo tarehe 20 mwezi Novemba, 2020 imemtia hatiani, mfanyabiashara wa Dawa za Kulevya ajulikanaye kwa jina la Yanga Omary Yanga maarufu ‘Rais wa Tanga’ na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kupatikana na Dawa za Kulevya aina ya Heroin Hydrochloride yenye uzito wa gramu elfu moja hamsini na mbili nukta sita tatu (1052.63 )
Baada ya kupitia ushahidi kwa ujumla wake Mahakama imebaini kuwa Jamhuri imefanikiwa kudhibitisha shtaka bila kuacha shaka hivyo kumtia hatiani Mshtakiwa huyo.
Shauri hili limeendeshwa na Mawakili wa Serikali Faraja Nchimbi, Pius Hilla, Salim Msemo, Constantine Kakula na Donata Kazungu.
Katika kudhibitisha shitaka hilo upande wa Jamhuri uliwaita mashahidi saba (7) na kutoa vielelezo nane (8) ambapo upande wa utetezi Mshtakiwa alijitetea mwenyewe na hakuwa na kielelezo chochote.
Mshtakiwa Yanga Omary Yanga alikamatwa Oktoba 1,2018 na Maafisa wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya baada ya kupekua nyumba yake iliyopo Mkoa wa Tanga eneo la Bombo na baada ya kukutwa na dawa hizo mshtakiwa alishtakiwa kwa kosa la Kusafirisha dawa za Kulevya chini ya kifungu cha 15 (1)cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya.