Aleksander Ceferin alisema Alhamisi kuwa hatawania muhula wa nne kama rais wa UEFA mnamo 2027 licha ya kuidhinishwa kwa mageuzi yenye utata ambayo yatamwezesha kuongeza muda wake.
“Niliamua takriban miezi sita iliyopita kwamba sitapanga kugombea tena 2027,” Ceferin alisema katika mkutano na waandishi wa habari kufuatia Kongamano la UEFA huko Paris.
“Sababu ni kwamba baada ya muda, kila shirika linahitaji damu safi, lakini hasa kwa sababu nilikuwa mbali na familia yangu kwa miaka saba sasa.”
Tangazo la Ceferin lilikuja muda mfupi baada ya mataifa wanachama wa UEFA kupiga kura kwa wingi kuunga mkono msururu wa marekebisho ya sheria, ikiwa ni pamoja na hatua ambayo ingemruhusu Ceferin kusalia katika nafasi yake hadi 2031.
“Kwa makusudi sikutaka kufichua mawazo yangu hapo awali, kwa sababu kwanza, nilitaka kuona sura halisi ya baadhi ya watu na niliiona,” alisema Ceferin, aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2016 kufuatia anguko la Mfaransa Michel Platini.
“Nina maisha mazuri katika soka, nina maisha mazuri nje ya soka pia.”