Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alielezea wasiwasi wake Jumatano jioni juu ya hasara kubwa ya maisha kati ya raia huko Gaza.
Taarifa kutoka Ikulu ya Elysee imesema Macron alijadili hali ya Gaza na eneo hilo katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Ilisema Macron aliwasilisha wasiwasi wake kwa Netanyahu kuhusu idadi kubwa ya vifo vya raia huko Gaza huku kukiwa na mzozo uliokithiri na hali ya dharura ya kibinadamu.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa Macron amemkumbusha Netanyahu wajibu wa Israel kuwalinda raia na kusisitiza udharura wa kuwasilisha misaada muhimu kwa raia wa Gaza.
Ilisema Macron alitetea juhudi za kusitisha mapigano kwa kudumu kwa usaidizi wa washirika wa kimataifa na kikanda, na kuongeza kuwa Ufaransa pamoja na Jordan zitafanya operesheni za misaada ya kibinadamu huko Gaza katika siku zijazo.
Kiongozi huyo wa Ufaransa pia alisisitiza haja ya Israel kuchukua hatua za kukomesha ghasia zinazofanywa na walowezi wa Kiyahudi dhidi ya raia wa Palestina na kusitisha miradi mipya ya makazi katika Ukingo wa Magharibi, akisema hali hii inatishia suluhu la mataifa mawili.
Macron pia aliwasilisha ujumbe kwa Iran na makundi tanzu yake kujiepusha na mzozo huo ili kuuzuia kuenea katika eneo hilo na kusisitiza umuhimu wa kutekelezwa kikamilifu kwa azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.