Rais wa Uganda Yoweri Museveni amepuuzilia mbali wasiwasi wake kuhusu kuondolewa kwa nchi yake katika mpango maalum wa kibiashara wa Marekani na Afrika,AGOA.
Wiki iliyopita, Rais wa Marekani Joe Biden alisema Uganda na nchi nyingine tatu za Kiafrika zitaondolewa kwenye mkataba wa (Agoa), akitoa mfano wa Uganda kama “ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu zinazotambuliwa kimataifa”.
Lakini Rais Museveni siku ya Jumapili aliikosoa Marekani, akisema “wanajiona bora kupita kiasi” na “kimakosa wanafikiri kwamba nchi za Afrika haziwezi kusonga mbele bila uungwaji mkono wao”.
“Kama Uganda inavyohusika, tuna uwezo wa kufikia malengo yetu ya ukuaji na mabadiliko, hata kama baadhi ya wahusika hawatuungi mkono,” aliongeza.
Marekani ndiyo ya hivi punde kuchukua hatua dhidi ya Uganda, ambayo mwezi Mei ilipitisha sheria tata ya kupinga mapenzi ya jinsia moja ambayo inajumuisha hukumu ya kifo kwa baadhi ya vitendo vya mapenzi ya jinsia moja.
Sheria hiyo iliifanya Benki ya Dunia kuondoa ufadhili wa Uganda,.
Alisema kuwa Uganda bado inaweza kujiendeleza bila msaada wa benki hiyo.
Rais Museveni, hata hivyo, alipongeza serikali ya Marekani kwa kudumisha ufadhili wa dawa za VVU, lakini akaongeza kuwa serikali yake ina mpango wa dharura wa kupata dawa hizo ikiwa wafadhili wa kigeni watajiondoa.